upenu2upenu2

INSHA ZA AWALI
KUJIFUNZA UPENDO

Gamier Mwaikoma

26 de septiembre 2013

Lugha ni zana ya kuelewa maana, au ituwezeshayo kufanya hivyo. Lugha inatupa maana ya mambo kwa kutumegea dhana ya vitu husika. Sasa kuko kanuni mbalimbali kuhusu ufahamu wa maana, moja wapo ni ile ya kutofautisha. Zoezi la Maana linajumuisha viungo shikika na vile dhahania, mara nyingi watu hupendelea sana kutegemea vitu shikika, vionekanavyo kuweka misingi ya maana zao, mfano  katika maendeleo ya ufahamu wa mtoto, ambapo kuna wakati huwa mdadisi, akivunja vitu na kujiumiza! Wazazi hukasirika lakini mtoto ndio anajifunza. Kwa mfano anaposhika moto akaungua, anajua huu ni moto, na ndio inapokuja hoja ya kutofautisha, baina ya poa, baridi, moto na joto, wakati mtoto hana kauli huwaachia wamzungukao maswali kuhusu maana ya hisia zake, mfano aliapo, pia kutoka lugha ya mwili wake, kama anatatizo lolote lile. Sasa tunapozungumzia kanuni ya maana kwa mujibu wa kutofautisha tunaangalia nguzo za ukinzano, mfano mchana kutoka katika usiku, asubuhi, jioni, mwanamke kutoka mwanaume, mtoto kutoka mkubwa, maskini kutoka tajiri, shibe kutoka njaa n.k. Wengine husema kinyume cha mambo! Lakini tunawajibika kuwa makini hapa , si kila kinyume tukichukuliacho jumla jumla, mara zote hulenga dhana ya maana husika, hapa sasa ndipo inapozuka haja ya ujifunza maana kwa kila namna iwezekanavyo, kupitia zana zote, lugha ikiwa moja, lakini si pekee…!Si jambo la ajabu kukuta mtu haelewi jambo fulani, hakuna mwenye kuelewa yote.., ni muhimu kuchukua tahadhari, na kuyachungua mambo zaidi ya sura yake ionekanayo, au dhaniwayo n.k. Sasa tunayapanga mambo kwa namba, namba ni mfumo wa asili wa kupangilia viwango, au thamani. Zoezi lakujifunza maana huanzia tumboni, kuendelea mara mtoto azaliwapo, na kuendelea siku zote…mpaka kifo, na baada (utaijua mwenyewe maana huko uendako) hujui vyote, hupewi vyote, kila kitu kwa umri husika, kuna hatari ya kuchanganywa ukipewa taarifa kupindukia, lakini pia kuna hatari ya kutapia mlo, kwa kunyimwa taarifa husika kwa wakati. Kuna maneno tumeyazoea sana, twayatumia kila leo, lakini muulize mtu sasa, maana yake, wengi wetu hatujui..! Au tunayachukulia rahisi tu, lakini yana maana pana zaidi kuliko upeo wetu. Mujibu wa pili wa kanuni ya maana ni ule wa kiwango cha neno lenyewe, kwa kuchungua mzizi wake.Mwenye maana nzuri ni yule mwenye kujua maana mbalimbali kwa nafasi zake husika. Kwa vipa umbele vyake..mambo ya kwanza, sehemu yake…yanayofuata na ya mwisho. Unaweza ukaishi miaka hata mia mbili, nabado usijue mambo madogo tu, na maana za msingi, au unaweza ukawa msomi na mtaaluma gwiji, lakini ukawa huna maana! Kwa kuanzia tupeane maana ya maisha, maisha ndio yanaleta haja ya maana,pasipo maisha what is the point?ni nini hoja ya maana, tunahitaji maana kwa kuwa tunaishi, na si vinginevyo! Sasa liangalie neno lenyewe Ma-ish-a; mzizi wake ni kiambishi ish-a, dhana ya kuisha, kinachokwisha, chochote kiishacho kina jinsi na kiwango…! Na zaidi kabisa kina chanzo, na hivyo mwisho.Kwa hivyo maisha , yanayokwisha, maana yake ni tuyatumiapo yangalipo. Kukukazia  hii hoja tuangalie neno upendo, msingi wa kwanza wa maana ya maisha..kinyume cha upendo si chuki, bali choyo, maisha si yako binafsi, maana ya maisha haitenganishwi na wengine, uishio nao, unaishi,au upo kwa ajili ya wengine, na wao kwa ajili yako wewe. Ndio sababu ni kikwazo sana kukosa wazazi, au walezi kwa mapana yake, tunatoa maisha yetu kwa ajili ya wanetu, na kuna wakati wao wanayatoa kwa ajili yetu, kwa mujibu huu huu tunaishi kwa ajili  wengine, na wao wanaishi kwa ajili yetu, sasa mtu anapokuwa mchoyo, anajiona yeye tu, au anataka wote waone kama yeye tu, hathamini, wala hatambui ya wengine,upendo ni pamoja na adili, huwezi kwa mfano kutumia njaa ya mtu, ukataka kumdhalili ili umpe chakula! Au mwalimu kumlala mwanafunzi, ili amfaulishe mtihani, ua kulewa katika eneo la kazi, au kutaka malipo yasiyo halali kufanya wajibu wako kwa jamii n.k. Hivyo tunafika kwenye nguzo ya pili ya maisha, heshima, heshima, si kwa watu au vitu fulani, bali kwa maisha kwa ujumla, watu hawaheshimu miili, mioyo, akili,mazingira,wenzao, n.k. Sasa ni jambo la huzuni kama utaishi maisha bila kujua mambo haya ya msingi ya maisha. Unaweza kuliona jambo kwa kutokuwepo kwa lingine, kwa mfano wewe unawabagua wenzako kidini leo, kwa sababu uko huru! Wakati usipokuwa huru hungefanya, wala hukufanya hivyo. Uhuru na amani ndio vimekufikisha hapo sasa,, unageuka na kusema mimi ni mkristo, mimi ni mwislamu, mpagani, au mwanadini za asili n.k. Ulipokuwa ukipigania uhuru wako ulikuwa na maana halisi ya maisha, ambao ndio msingi wetu wa mwisho: Utu, ulikutana na wenzio kwa sababu ya utu, sasa badala ya kujenga kwenye misingi uliyoachiwa unabomoa…matokeo yake utaupoteza uhuru wako tena, kisha utajifanya umekuwa mtu tena…, ukishapata shida, kwa nini usiendelee kuwa mtu, kwa kuthamini utu? Pengine inatubidi turudi kwenye namba za msingi, tujifunze upya upendo.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s